Rais ateua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, viongozi mbalimbali

0
157

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Jacob Casthom Mwambegele aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Jaji Mwambegele anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Semistocles Kaijage ambaye amemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais pia amemteua Jaji Mwanaisha Athuman Kwariko kuwa mjumbe wa tume hiyo.

Jaji Kwariko anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Jacob Casthom Mwambegele.

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji Sam Mpaya Rumanyika, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Taarifa hiyo imeeleza pia Rais amemteua Profesa Khamis Dihenga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Kabla ya uteuzi huo Profesa Dihenga alikuwa anahudumu kwa Mkataba katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Morogoro.

Profesa Dihenga anachukua nafasi ya Profesa William Anangisye aliyemaliza muda wake.

Rais Samia pia amemteua Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Mussa Muhidin Kissaka, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambapo uteuzi wa viongozi hao umeanza Desemba 23, 2021.