Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinafanya jitihada kubwa ili kuwafanya wavuvi wawe na uhakika wa kupata samaki pindi wakienda majini badala ya kuwinda kama wanavyofanya hivi sasa.
Ulega ameyasema hayo kwenye hafla ya kuwakabidhi wavuvi vifaa maalum vitakavyowawezesha kutambua maeneo yenye samaki kabla ya kuingia majini na kuanza shughuli ya uvuvi iliyofanyika jana Shehia ya Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja (Zanzibar)
“Kwanza nimefarijika kuona wavuvi wengi kwenye shehia hii ni vijana hivyo nina uhakika itakuwa rahisi wao kutumia vifaa hivi na kuwafundisha wazee ambao bado wanaendelea na shughuli za uvuvi kwa hapa Kusini Unguja” Ameongeza Ulega.
Ulega ameiagiza Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo ili wavuvi hao waanze kuvitumia ambapo ametoa rai kwa wavuvi kutumia vizuri teknolojia hiyo.
Ulega ameongeza kuwa hatua ya kugawa vifaa hivyo itaendelea kuchochea kampeni ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha pande hizo zinaingia kwenye uchumi wa buluu jambo ambalo ameweka wazi kuwa litainua uchumi wa wavuvi kwa kiasi kikubwa.