Maabara za kupima UVIKO-19 zimethibitishwa na WHO

0
176

Maabara za Tanzania zina uwezo wa kupima UVIKO-19 na majibu yake yana ubora unaokubalika kikanda na kidunia kwa mujibu wa taarifa ya EAC na Vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO)

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe wakati wa ziara maalum ya kukagua mwenendo wa huduma za upimaji wa UVIKO-19 ndani ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA)

Dkt. Sichalwe amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi 6 za Afrika Mashariki ambayo maabara zake zimefanyiwa utambuzi na kukubalika na jumuiya hiyo.

Katika Taarifa ya ya tathmini ya Ubora wa Huduma za upimaji wa UVIKO-19 iliyowasilishwa mwezi Novemba na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maabara ya Taifa imepata asilimia 100 ya vipimo vya Ubora huku Maabara nyingine za Kanda zikiwa zimepata asilimia 96-98 kiwango ambacho ni Cha juu ukilinganisha na kiwango Cha asilimia 80 kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)

Hata hivyo amesema kuwa Wizara kupitia Maabara kuu ya Taifa ya Jamii imefunga mashine nyingine kubwa na za kisasa kwa ajili ya kupima kipimo cha haraka cha UVIKO-19(PCR ) kwa wasafiri wanaoenda nchi za Falme za Kiarabu ikiwemo Dubai.

“Nimefika hapa uwanja wa ndege kujionea hali halisi na hali ni nzuri, mashine za kutosha zipo na timu inaendelea na kazi na pia nimeshuhudia eneo la tenti nje ya uwanja ambapo wateja watakapokuwa wanaanzia kupatiwa huduma. Kikubwa wafike mapema na kwa wakati kulingana na muda wa safari zao.” alisema Mganga Mkuu Dkt. Sichalwe.

Kwa upande wake, Meneja wa huduma za afya mipakani, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa huduma za afya katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Remidius Kakuru ameeleza kuwa, Wizara imeendelea kupima wasafri wanaoingia na wanaotoka nchini na zoezi linaenda vizuri.

“Niwasisitize wasafiri kuwa, huduma imeanza kutolewa tokea tarehe 16 mwezi huu na tayari tunaendelea na upimaji kwa wasafiri wanaokwenda Dubai.

Tunawasisitizia wasafiri wajitahidi wafike mapema uwanja wa ndege ikiwezekana masaa saba kabla ya safari zao na gharama hizi za kipimo cha pili ni sawa na ile ya kipimo cha kwanza.” Amesema Kakuru.

Nae Mwandisi Barton Komba ambaye ni Meneja wa JNIA Terminal 3, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mashine hizo kwa haraka na abiria wote kuweza kupima ndani ya uwanja huo.

“Kwa niaba ya mamlaka ya viwanja vya ndege, tunapongeza juhudi za Serikali kwa kuwezesha kuletwa mashine ndani ya siku tatu na abiria wanapatiwa huduma na sasa ndege ya Emirates itaanza kuondoka kwenda huko Dubai na tutarudi kwenye shughuli yetu kama ilivyo awali.” Alisema Komba.

Katika kuhakikisha ndege hizo za Falme za Kiarabu zinaendelea na safari zake hapa nchini, Meneja wa ndege za Emirates Tanzania katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3, Aboubakar Juma amemhakikishia Mganga mkuu wa Serikali kuwa, Emirates itaendelea na safari zake ambapo kwa sasa wanasubiria kukamilika kwa taratibu za upimaji mara ya pili kwa wasafiri ndani ya uwanja huo.

Wasafiri wanatakiwa kufanya miahadi ya safari zao ‘booking’ kupitia mtandaoni katika;

https://pimacovid.moh.go.tz/#/booking na kufanya malipo na kisha kuchagua kituo cha kupima na kupata cheti ambacho kinakuwa tayari ndani ya masaa 48.