Expo 2020 Dubai fursa ya kuitangaza Tanzania

0
150

Naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema Tanzania itatumia fursa ya ushiriki wake katika maonesho ya Expo 2020 Dubai kutangaza maeneo ya uwekezaji pamoja na vivutio vya Utalii.

Balozi Mbarouk pia ametumia fursa hiyo kushauri namna bora ya kuandaa ‘Tanzania National Day’ ambayo imepangwa kufanyika Februari mwaka 2022.

Balozi Mbarouk Amesema,” Tujifunze kutoka kwa wenzetu ambao wameishaandaa shughuli zao ili na ya kwetu iwe ya aina yake. Tujipange na tujiandae vema ili tuhakikishe siku hiyo Tanzania inapata heshima yake”

“Kati ya nchi 192, tumepewa heshima ya kuwa miongoni mwa mataifa makubwa ulimwenguni kuwapo hapa leo, tuitumie nafasi hii kujijengea jina kubwa zaidi na kuonyesha fursa zinazoiweka Tanzania mbele kama moja ya nchi yenye maendeleo ya kasi”-amesisitiza Balozi Mbarouk

Aidha ameongeza kuwa maonesho hayo ni sehemu nzuri ya kujifunza, kupata uzoefu, kujitangaza, kuleta hamasa kubwa na kuchochea ukuaji na maendeleo ya Sekta mbalimbali kupitia mafanikio ya ushiriki wa Tanzania kwenye maonyesho hayo.