Aliyefariki na kuzikwa, apatikana akiwa hai

0
207

Mtoto Leornard Morisha mwenye umri wa miaka 11 anayedaiwa kufariki dunia Juni 27 mwaka 2017 na kuzikwa katika kijiji cha Ngemo wilayani Mbogwe mkoani Geita, amepatikana akiwa hai katika kijiji cha Segese wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe amethibitisha kupatikana kwa mtoto huyo na kusema kuwa baada ya kupatikana walimpeleka katika kituo cha afya cha Masumbwe kwa ajili ya kupimwa afya yake, ambapo amekutwa na afya njema lakini akiwa amekatwa ulimi.

Amesema mwezi Oktoba mwaka huu Leonard alionekana akizunguka zunguka usiku katika maduka yaliyopo mjini Kahama na ndipo akachukuliwa na mmoja wa walinzi katika maduka hayo ambaye alikwenda kumuhifadhi nyumbani kwake hadi alipopatikana.

Kwa mujibu kamanda Mwaibambe, tarehe 12 mwezi huu baadhi ya Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika kijiji cha Segese waliotokea kijiji cha Ngemo, ndio walimtambua mtoto huyo.

Amesema baada ya mtoto huyo kupatikana, jeshi la polisi mkoani Geita liliomba kibali cha kufukua kaburi lake na kufukuliwa tarehe 16 mwezi huu, ambapo walichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi.