Waziri Mkuu awataka UVCCM kukuza vipaji vya vijana

0
157

Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa ameushauri uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM) kuendelea na mshindano ya GREEN CUP kila mwaka Ili kuibua vipaji kwa vijana wengi wanaoweza kusaidia Taifa kwenye michezo.

Waziri Mkuu amesema hayo kwenye fainali za mashindano hayo ambayo yamejumuisha timu za umoja wa vijana kila mkoa.

Fainali za mpira wa miguu zimewakutanisha timu ya UVCCM mkoa wa mjini Magharibi na timu ya UVCCM mkoa wa Pwani ambapo mkoa wa Mjini Magharibi umeibuka bingwa na hivyo kuondoka na kikombe na donge nono la shilingi milioni 10, huku Mkoa wa Pwani ukiondika na milioni 5.

Mkoa wa mjini Magharibi umetwaa ubingwa huo baada ya kuitandika Pwani mabao 3-1.

Mashindano hayo pia yameshuhudia fainali ya mchezo wa Pete kati ya Dar es Salaam na Mkoa wa Mjini Magharibi.

Fainali hiyo imemalizika kwa Dar es salaam kuibuka na ushindi wa magoli 43 kwa 36 ya Mjini Magharibi.

Akimkaribisha Waziri Mkuu wakati wa kutoa zawadi hizo Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Kenan Kihongosi amesema mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vipya kwenye Michezo.

“Tumeweza kumaliza mashindano salama na kuibua vipaji kwa vijana, na mshindano haya yakiendelezwa tutaweza kupata vijana wenye vipaji ambao wanaweza kushiriki ligi kuu ya Tanzania na hata kimataifa”-Amesema Kenan Kihongosi

Mashindano ya UVCCM GREEN CUP yamefanyika kwa mara ya kwanza yakijumuisha timu za UVCCM mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kwa lengo la kuwaleta vijana wa CCM kuwa Pamoja kupitia Kimichezo.