TRA waonywa kufungia maduka ya wafanyabiashara

0
1437

Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango ameitaka Mamlaka ya Mapato Nchini TRA  kusitisha utaratibu wa kuwafungia wafanyabiashara, biashara zao ili kushinikiza alipe kodi anayodaiwa.

Waziri Mpango amesema hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya Uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo ameiagiza TRA  kumfungia biashara mfanyabiashara ambaye ni sugu kwa kukwepa kodi kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa Tra.

Aidha ameielekeza TRA kujikita zaidi kutoa elimu kwa mlipa kodi juu ya utunzaji wa vitabu vya hesabu za biashara, na kumpa fursa ya kufanya naye majadiliano kuhusu mpangilio bora wa kulipa malimbikizo ya kodi kwa mkupuo au kwa awamu pamoja na adhabu stahiki kama zilivyobainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Kodi 2015.