Rais Samia awaongoza Watanzania katika maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru

0
225

Rais Samia Suluhu Hassan, leo amewaongoza Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, katika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wastaafu wa Tanzania na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya viongozi kutoka nje ya nchi walioshiriki kwenye sherehe hizo ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Philipe Nyusi wa Msumbiji na Rais wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani.

Katika sherehe hizo Eswatini imewakilishwa na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Thema Masuku, Rais mstaafu wa Malawi Dkt. Joyce Banda ameiwakilisha Malawi, Burundi imewakilishwa na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Prosper Bazombanza, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imewakilishwa na Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde na Botswana imewakilishwa na Rais Mstaafu wa nchi hiyo Festus Mogae.

Sherehe hizo zimepambwa na burudani mbalimbali ikiwa ni pamoja na gwaride maalum kutoka vikosi vya ulinzi na usalama, burudani ya vijana wa halaiki walioonesha maumbo mbalimbali na maonesho ya ndege za kijeshi.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni miaka 60 ya Uhuru, Tanzania Imara, Kazi Iendelee.