Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar aongoza kongamano la kitaifa

0
138

Kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman amewakumbusha Watanzania kutafakari walikotoka na wanakokwenda.

Othman ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam, wakati akifunga kongamano la kitaifa la miaka 60 ya Uhuru lililoandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kuhudhuliwa na watu mbalimbali mashuhuri na Wanafunzi waliosoma na wanaoendelea kusoma chuoni hapo.

“Kongamano hili limetuamsha na kutukumbusha nchi hii imetoka wapi hasa katika masuala ya uongozi, lazima tujiulize kuwa tumefika hapa na miaka 60 ijayo tutakuwa wapi.” ameongeza Makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka 60, bado kuna changamoto ambazo Watanzania wanapaswa kukabiliana nazo wakishirikiana na Serikali ili kila mmoja apate huduma muhimu ikiwa ni afya, elimu na miundombinu iliyo bora.

Akichangia mada Katika kongamano hilo waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema kila Mtanzania ana haki ya kufurahia maendeleo ya Taifa yaliyopo na pia kuna umuhimu kwa kila Mwananchi kuona fahari ya maendeleo hayo.

“Kwa watu ambao tumeishi kipindi hiki maendeleo tuliyoyapata ni makubwa sana, ukiona maendeleo upande wa elimu na mambo mengine mengi ni makubwa sana, niseme tu tumepiga hatua kubwa lakini inabidi Wananchi nao waone mabadiliko hayo. ” amesisitiza Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba

Naye Mkuu wa chuo cha Taifa cha Ulinzi Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema lazima Watanzania hasa vijana wawe wazalendo kwa nchi yao kwa kulinda amani na utulivu uliopo, huku akisema vyombo vya usalama nchini vimejitahidi kuisimamia amani hiyo pamoja na kuwepo na changamoto kadhaa.