Wataka kutofautishwa ulemavu na ushirikina

0
173

Baadhi ya watoto wenye ulemavu wilayani Ileje mkoani Songwe wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi,  ili waweze kutofautisha ulemavu na mambo ya kishirikina.
 
Watoto hao wametoa ombi hilo wakati wa maadhimsho ya Siku ya Wenye Ulemavu Duniani yaliyofanyika kwa pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, yaliyofanyika kiwilaya wilayani Ileje.
 
Wamesema wazazi ama walezi wengi wamekuwa wakichelewa kutoa huduma stahiki kwa watoto wao wenye ulemavu wakiamini kuwa wamerogwa, hali inayochangia watoto wengi wenye ulemavu wilayani humo kutopata msaada.
 
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mkuu wa wilaya ya Ileje, Anna Gidary  amesema wilaya hiyo ina zaidi ya watoto mia mbili wenye ulemavu pamoja na shule tatu za watoto wenye ulemavu.
 
Baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki maadhimisho hayo ya Siku ya Wenye Ulemavu Duniani na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika kiwilaya wilayani Ileje wamesema,  watoto wenye ulemavu ni sawa na watoto wengine hivyo wazazi hawapaswi kuwatenga.
 
Katika hatua nyingine Wakazi wa wilaya ya Ileje wamefanya usafi katika eneo linalotarajiwa kujengwa shule ya msingi ya Ipala ambapo tayari Serikali imetoa shilingi milioni 400 ili kukamilisha ujenzi huo.