Rais John Magufuli ameagiza wastaafu wote waliofikia umri wao wa kustaafu kulipwa kulingana na kikotoo kilichotumika katika mifuko yao ya hifadhi ya jamii kabla mifuko hiyo haijaunganishwa kwa kipindi cha mpito hadi mwaka 2023.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar Es Salaam kwenye mkutano na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na viongozi wa serikali ambapo amesema kustaafu ni heshima hivyo wafanyakazi lazima waheshimiwe kutokana na kufanya kazi kwao.
“Nimeamua kuanzia leo wastaafu wote walipwe kwa kikotoo kilichokuwepo cha zamani kwenye mifuko yao na si vinginenvyo na baadae ndio yaletwe mapendekezo mapya ya kikokotoo kilicho bora na si kwa sasa kwa kuwashtukiza wastaafu ambao wamefanya kazi kwa heshima”alisema Rais Magufuli.
Amesema katika kipindi cha mpito ana uhakika msimamizi wa mifuko pamoja na serikali wataweza kukaa pamoja na kushirikiana kuwa na kikotoo ambacho kitakuwa bora na chenye kuridhisha pande zote.
Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wote nchini kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha malengo yanatimia na kusaidia maendeleo hapa nchini.
