29 wathibitika kufa maji

0
303

Watu 29 wamethibitika kufa maji nchini Nigeria baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika jimbo la Kano.
 
Wakati boti hiyo inazama ilikuwa imebeba idadi kubwa ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka kwenye kijiji cha Badau kwenda mji wa Bagwai kushiriki kwenye shughuli ya kidini, huku wengi wao wakiwa ni Wanafunzi.
 
Habari zaidi kutoka nchini Nigeria zinaeleza kuwa zoezi la kutafuta miili zaidi ama watu walionusurika kifo linaendelea, likishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.
 
Wazazi na Walezi wa Wanafunzi waliokuwa wakisafiri na boti hiyo pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa abiria wengine waliokuwa wakisafiri na boti hiyo wamekusanyika katika eneo ilipotokea ajali hiyo, kwa lengo la kusubiri taarifa za wapendwa wao waliopatikana wakiwa hai ama wamefariki dunia.
 
Mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika,  na mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi.
 
Ajali za vyombo vya majini zimekuwa zikitokea mara kwa mara nchini Nigeria, huku sababu zikitajwa kuwa ni pamoja na vyombo hivyo kupakia abiria zaidi ya uwezo wake, kutofanyiwa matengenezo kwa vyombo hivyo na kutokuwepo kwa usimamizi madhubuti kwa vyombo hivyo vya majini.
 
Mwezi Mei mwaka huu zaidi ya watu mia moja walifariki dunia nchini Nigeria baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama  katika jimbo la Kebbi,  na wiki mbili zilziopita wasichana saba walifariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama karibu na jimbo la Jigawa.