Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali itaendelea kuwekeza na kuchukua hatua za makusudi kukuza sekta ya utalii nchini.
Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii jijini Arusha mara baada ya kuzindua hoteli ya nyota tano ya Gran Melia Hotel.
Amewaeleza wadau hao kuwa asilimia 5 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya uhifadhi, na kutokana na wingi wa vivutio vya kitalii vilivyopo nchini, inaaminika kwamba Safina ya Nuhu anayeelezwa kwenye Biblia iliishia Tanzania.
Awali akizungumza kuhusu sekta ya utalii nchini, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa serikali imetenga TZS bilioni 92.2 kwa ajili ya kukuza sekta hiyo baada ya kuathiriwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19).
Amesema kuwa tangu Januari 2021 watalii wameongezeka kwa asilimia 52 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2021/22, Waziri Ndumbaro amesema kwamba watalii wameongezeka kwa asilimia 248 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020, mafanikio ambayo yametokana na chanjo ya UVIKO19.
Kwa upande wa Uongozi Gran Melia Hoteli ametoa ahadi kwa Rais Samia ya kuwekeza zaidi nchini kwa kujenga hoteli za kisasa ambazo zitavutia watalii zaidi.
Hadi sasa wawekezaji hao wana hoteli sita nchini Tanzania ambazo zimetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 800 na wanatarajia kuwekeza zaidi.