Chongolo: Kazi ya Siasa sio uongo na Majungu

0
168

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuendekeza uongo, fitina, majungu, umbea na kusingiziana ambapo amewakumbusha kuwa, kazi ya siasa ni kusemeana mema, kupendana na kushikamana.

Chongolo ameyasema hayo katika muendelezo wa ziara yake na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoa wa Kagera akiwa wilayani Muleba katika kikao cha shina namba 05 tawi la Lulanda.

“Kazi ya siasa sio uongo, kazi ya siasa sio majungu, sio fitina, sio umbea wala sio kusingiziana, Kazi ya siasa ni kuombeana mema, kazi ya siasa ni kupendana, kushikamana, kazi ya siasa ni kuneneana mema wenzio.”-amesema Chongolo.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu imekuja baada ya kupokea taarifa ya viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo walionza kusemana vibaya na kujengeana fitina ikiwa ni maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama mapema mwakani.

Katika hatua nyingine, Chongolo amezitaka serikali za mikoa na wilaya zinazopakana na ziwa victoria kuendeleza jitihada za kupambana na uvuvi haramu katika ziwa hilo.

Katibu Mkuu amesema, madhara ya uvuvi haramu katika ziwa hilo ni makubwa na kwamba serikali ikiacha kudhibiti matendo hayo, uvuvi haramu utaendelea kutengeneza mazingira magumu kwa mikoa hiyo na wananchi kunufaika na uchumi unaotokana na ziwa hilo.