Waziri Ally: Wananchi wanahitaji elimu ya Kifedha

0
166

Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Jamal Kassim Ally, amezitaka taasisi za fedha kutumia wiki ya  maonesho ya huduma za kifedha yanayoendelea jijini Dar es Salaam, kutoa elimu kwa wananchi itakayokwenda kutatua changamoto za kutofikiwa na huduma za fedha ikiwemo elimu ya fedha, mikopo na bima.

Ameeleza hayo jijini Dar es Salaam leo wakati akizindua wiki ya  maonesho ya huduma za kifedha iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa programu ya uelimishaji wa nyenzo ya ufundishaji wa elimu ya fedha katika maeneo yote nchini na kufafanua kuwa asilimia 8.6 ya wananchi waishio mijini ndio wanaofikiwa na huduma za kifedha ipasavyo.

“Katika kukuza na kupunguza umasikini, Serikali Katika mpango wa Taifa wa mwaka 2021/22 na 2025/26 tumepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 133.3 katika sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati katika kukuza na kuendeleza uchumi wa watanzania,”-ameongeza Waziri Ally.

Aidha Waziri Ally amezitaka taasisi hizo zijitathmini baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo kwa kupata idadi ya wananchi na wangapi wameongeza ufahamu wa matumizi ya fedha, wajasiriamali  wangapi wameunganishwa na fursa na uelewa wa kutumia huduma rasmi na huduma zipi zimesogezwa karibu na jamii.

Kwa upande wa baahi ya taasisi za kifedha zikiwemo sekta za benki, mitandao ya simu, na bima wamesema watatumia maonesho hayo kuhakikisha wanafikisha elimu ya kifedha kwa wananchi ili sekta hizo za kifedha ziweze kuongeza tija kwenye ukuaji wa uchumi.