Bilioni 50 kuanzisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko

0
166

Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 50, kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya uvuvi ambayo itajengwa wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa makabidhiano ya eneo hilo la mradi kwa mshauri Elekezi wa kampuni ya Sering kutoka nchini Italia, kwa ajili ya kukamilisha kandarasi ya upembuzi yakinifu utaopelekea kujulikana kwa gharama za mradi huo na kutangaza zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo.

Dkt. Tamatamah amesema kuwa, ujenzi wa bandari ya uvuvi ni moja ya mkakati wa serikali katika kuhakikisha inaendelea kukuza sekta ya uvuvi hasa katika kuhamasisha uwekezaji na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa.

“Ujenzi huu wa bandari ya uvuvi unakwenda sambamba na ununuzi wa meli mbili (2) kubwa za uvuvi ambazo zitafanya uvuvi katika bahari kuu lakini Serikali pia inalifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo ndilo litakalokuwa likisisimamia meli hizo,” amesema Dkt. Tamatamah

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainabu Kawawa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo na kuhakikisha wanaanza kujipanga kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwepo wa mradi huo.