Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen ameagiza kuitishwa kwa baraza la dharura la Halmashauri ya wilaya ya Ulanga kujadili taarifa ya Tume iliyoundwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa shilingi Bilioni 2.9 zinazodaiwa kutumika kinyume na utaratibu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Morogoro, Dkt. Kebwe pia ameagiza aliyekuwa mhasibu mkuu wa halmashauri hiyo Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa wilayani Gairo kurejea mara moja wilayani Ulanga ili kujibu tuhuma hizo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhusu matumizi ya fedha za serikali huku akimuelekeza Katibu Tawala wa mkoa huo kufuatilia utekelezwaji wa maagizo ya Tume hiyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi anaeshughulikia serikali za mitaa Noel Kazimoto amesema hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika na makosa hayo.
