Daktari mmoja aliyejulikana kwa jina la Karim Bakari kutoka kijiji cha Maheha wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara anashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo kwa kosa la kutoa huduma za upasuaji na matibabu kwa wagonjwa nyumbani kwake kinyume na taratibu.
Daktari huyo ambaye alifukuzwa kazi mwaka jana katika hospitali ya wilaya ya Newala kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mgongwa aliyefanyiwa upasuaji amesema aliamua kufanya hivyo kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa nao na kuomba serikali imsamehe.
Mkuu wa wilaya ya Tandahimba Kanali Patrick Sawala amesema kukamatwa kwa daktari huyo kutokana na uchunguzi uliofanywa kwa muda mrefu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Kanali Sawala ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kufuata hatua za kisheria na kufuatilia kwa kina wapi ambako alikuwa akipata dawa na vifaa tiba ambavyo vilikuwa vinatumika wakati anatoa huduma nyumbani kwake huki akionya wale wanaoendelea kufanya hivyo katika wilaya yake kuacha mara moja.
Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Tandahimba Daktari Silas Sembiko amewataka wananchi kuacha tabia ya kupata huduma za afya vichochoroni kwani ni hatari kwa afya zao.