Ujerumani imeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 71 sawa na shilingi bilioni 190.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, afya ya mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Nyaraka za makubaliano ya msaada huo zimesainiwa mkoani Dar es Salaam kati ya Naibu Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje Amina Khamis Shaaban na kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Ujerumani Marcus Von Essen.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa nyaraka hizo, Naibu Katibu Mkuu Amina Khamis Shaaban ameyataja maeneo yatakayonufaika na msaada huo kuwa pamoja na afya ya mama na mtoto iliyotengewa Euro milioni 24 na mradi wa kuzuia migogoro baina ya wanyamapori na binadamu utakaotumia Euro milioni 6.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje ameishukuru Ujerumani kwa kuanzisha majadiliano na Tanzania baada ya kuyasitisha mwaka 2015, na kuahidi kuwa fedha zitakazotolewa zitatumika ipasavyo na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Regine Hess na kiongozi wa ujumbe wa Ujerumani ulioshiriki majadiliano yaliyofanikisha kupatikana kwa msaada huo Marcus Von Essen, wamesema Ujerumani imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita.
Wamesema chini ya makubaliano mapya, Ujerumani itajikita zaidi kusaidia afya ya mama na mtoto, kusaidia masuala ya bima ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), maji na usafi wa mazingira, usimamizi wa fedha za umma, kuhifadhi maeneo ya urithi wa dunia kama vile hifadhi ya Selous na kuwalinda Wanawake na Wasichana dhidi ya vitendo vya kikatili.