Klabu ya Simba imesema imeridhia ombi la aliyekuwa Kocha wake Mkuu, Didier Gomes da Rosa la kuachana na timu hiyo kuanzia leo Oktoba 26, 2021.
Taarifa klabu ya Simba kupitia mtandao wao wa Kijamii wa Instagram imesema baada ya tathmini na majadiano ya kina, pande zote zimeafikiana kwa mujibu wa mkataba na manufaa ya wote.
Taarifa hiyo imeeleza, kutokana na hatua hiyo, aliyekuwa Kocha Msaidizi Thierry Hitimana, ndiye atakuwa Kocha Mkuu wa Simba katika kipindi hiki cha mpito akisaidiwa na Selemani Matola.
Aidha, Klabu pia imefanya mabadiliko madogo katika benchi la ufundi kwa kusitisha mikataba ya aliyekuwa Kocha wa Makipa, Milton Nienov na Kocha wa Viungo, Adel Zrane.
Kusitishwa kwa Makataba wa Gomes kunakuja ikiwa zimepita siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana walipokubali kichapo cha mabao 3-1, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Gomes alitua nchini akichukua nafasi ya aliyekuwa Kocha wa kikosi hicho Mbeligiji Sven Van de broeck aliyetimkia Far Rabat ya Morocco.