Wasanii watakiwa kusajili kazi zao

0
221

Serikali imetoa wito kwa wasanii kuendelea kusajili kazi zao katika mamlaka zinazo husika ili zilindwe kisheria na mamlaka hizo katika kuhakikisha zinawanufaisha na kufanikisha ndoto zao.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa wakati akijibu maswali ya baadhi ya Wabunge waliotaka kujua msimamo wa Serikali katika kudhibiti wizi wa kazi za sanaa kupitia ombwe kubwa la uwepo wa teknolojia zinazowawezesha wezi kudurufu kazi za wasanii na kuziuza bila kibali cha msanii husika.

Katika kikao hicho baina ya watendaji wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma, na Maendeleo ya Jamii, Waziri Bashungwa amewaelezea wajumbe kuwa nia ya Serikali ni kuona vijana wananufaika kupitia kazi zao, lakini kwa kufuatasSheria za nchi, kanuni, taratibu na miongozo zilizowekwa kwa lengo la kulinda masilahi yao.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizira ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara hiyo inaendelea na uratibu kuona namna bora inavyoweza kuwapeleka wataalamu wa sanaa nje ya nchi kujifunza na kuongeza ujuzi zaidi ili baadaye warejee hapa nchini kuwasaidia wasanii na hasa wasanii wachanga kuzalisha kazi zenye ubora zaidi.