Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imekiri kupata taarifa za tatizo la upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo unaosababishwa na msukumo mdogo kutoka katika chanzo cha maji cha Ruvu Chini.
Dawasa imesema tatizo hilo limesababishwa na upungufu wa maji katika mitambo ya kuzalisha maji ambayo imelazimu mamlaka kupunguza uzalishaji maji kutoka lita milioni 270 hadi lita milioni 210 kwa siku.
Uwezo wa kuzalisha maji kwa siku ni lita milioni 520, hata hivyo kutokana na upungufu wa maji katika chanzo cha mto Ruvu, Dawasa inazalisha lita milioni 460 sawa na upungufu wa lita milioni 60 kwa siku.
Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema DAWASA kwa kushirikiana na Ofisi za Bonde la Wami Ruvu wanaendelea na zoezi la kusitisha matumizi ya maji kwa watumiaji wengine katika mto huo ikiwa ni pamoja kusitisha vibali vya umwagiliaji ili kuruhusu maji kufika mitamboni.
“Ili kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa usawa katika eneo linalohudumia na mtambo wa Ruvu Chini, DAWASA imehamisha sehemu ya maji ya Ruvu juu ili yatumike kwa maeneo yaliyokuwa yanahudumiwa na Mtambo wa Ruvu Chini,”- Ameongeza Luhemeja.