Katibu Mkuu CCM aelekeza kamati za Siasa na Wizara kusimamia mgawanyo wa fedha za UVIKO-19

0
215

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ametoa maelekezo kwa Kamati za Siasa za Mikoa na Wilaya nchi nzima kuhakikisha zinasimamia fedha za UVIKO 19 shilingi Trilioni 1.3 zinazopelekwa katika maeneo yao, sambamba na wizara zote kuweka mgawanyo wa wazi wa fedha hizo kama ilivyofanyika Katika wizara ya TAMISEMI.

Katibu Mkuu ametoa maelekezo hayo katika ziara ya kikazi ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Samia Suhulu Hassan Mkoani Arusha.

“Kamati zote za siasa ngazi za Mikoa na Wilaya nchi nzima, popote pale fedha zitakapothibitika zimepotea na ninyi mtawajibika kwa kutosimamia fedha hizo kwenye maeneo yenu, kwa sababu, kwa kutofanya hivyo tutakuwa tunaikwamisha Ilani yetu wenyewe kutekelezwa katika kiwango chenye tija.” Katibu Mkuu CCM Ndg. Chongolo

Wakati huo huo, Katibu Mkuu ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kutoa mchanganuo wa fedha za UVIKO 19, ilizopokea katika mgao wa kila wizara ambapo amezitaka wizara zote kutoa mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kwa kufuata mfano ilivyofanyika kwa wizara ya TAMISEMI inayoongozwa na Ummy Mwalimu.

Aidha, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na kuwaomba wanaArusha na watazania wote kuendelea kumuunga mkono Rais Samia pamoja na Serikali anayoiongoza kwani imedhamiria kufanya mambo makubwa na yenye tija kwa wananchi wote.