Hukumu ya kesi ya kina Aveva yaahirishwa

0
172

NA, Emmanuel Samwel, TBC

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo mkoani Dar es Salaam, imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya kughushi na kula njama inayomkabili aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba Evansi Aveva na mwenzake hadi tarehe 21 mwezi huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Thomas Simba kueleza kwamba hajamaliza kuandika hukumu ya shauri hilo, hivyo kulazimika kupanga tarehe nyingine kwa ajili kutoa hukumu ya shauri hilo.

Hata hivyo mshtakiwa Aveva hakuweza kufika mahakamani hapo wakati kesi hiyo ikitajwa kwa kile kilichodaiwa na mshtakiwa namba mbili Godfrey Kaburu kuwa mwenzake amekwenda hosiptalini kwa ajili ya kuangalia afya yake.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo mbalimbali pamoja na mashahidi 10, huku washtakiwa wakijitetea wenyewe.

Mahkama hiyo iliwakuta washtakiwa Evansi Aveva na wenzake na kesi ya kujibu katika mashtaka manne likiwemo la kula njama, kughushi nyaraka na kutoa maelezo ya uongo.

Katika shtaka la kughushi, washtakiwa wote wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Klabu ya Simba zina thamani ya dola 40,577 za Kimarekani, sawa na zaidi ya shilingi milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli kosa ambalo wanadaiwa kulitenda Mei 28 mwaka 2016 mkoani Dar es Salaam.

Pia katika mashtaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe ambaye sasa ni marehemu kati ya Machi 10 na Septemba 30 mwaka 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo wakionyesha kwamba Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577 wakati wakijua sio kweli.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi hiyo hadi tarehe 21 mwezi huu kwa ajili ya kutoa hukumu ya shauri hilo.