Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Watumishi watatu wa halmashauri wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kwa tuhuma za upotevu wa mapato.
Waziri Mkuu Majaliwa amewasimamisha kazi Watumishi hao wakati wa mkutano wake na Watumishi, Madiwani pamoja na Wananchi wa halmashauri wilaya ya Kilwa.
Watumishi hao ni kutoka idara ya mapato ambao ni Bahaye Shilungushela, Mohamed Samadu na Ally Kinyonge.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema mapato mengi yanayokusanywa katika wilaya ya Kilwa hayapelekwi benki, na badala yake Watumishi hao wamekuwa wakitumia fedha hizo kwa matumizi binafsi.
Hatua hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa imekuja baada ya Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) wilaya ya Kilwa na mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria Watumishi hao baada ya Baraza la Madiwani la halmashauri ya Kilwa kubaini upotevu wa mapato na kushauri vyombo vya dola kuchukua hatua.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Mweka Hazina wa wilaya ya Kilwa, Mudrika Mjungu kurekebisha mashine 55 za kielekroniki za kukusanya mapato, ili ziweze kufanya kazi.