Ndaki atatua kero ya wafanya biashara ya dagaa

0
137

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka maofisa uvuvi kuacha kuwatoza ushuru wa kusafirisha mazao ya uvuvi nje ya nchi wafanyabiashara wa dagaa wanaofanya biashara hiyo katika soko la ndani ya nchi.

Ametoa maagizo hayo jana wakati akiongea na wafanyabiashara wa dagaa katika mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe akiwa katika ziara yake ya siku mbili, ambapo wafanyabiashara hao wamedai kuwa wamekuwa wakitozwa ushuru huo wakati baadhi yao hawasafirishi dagaa nje ya nchi.

Waziri Ndaki amesema wafanyabiashara wanaopaswa kutozwa ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi ni wafanyabiashara wa dagaa ambao hununua na kuuza kwenye masoko yaliyopo nje ya Tanzania ambapo kwa Tunduma huuzwa zaidi nchi za Zambia na Congo.

“Tuache mara moja kuwatoza wafanyabiashara wa dagaa ambao wanauzia kwenye soko la ndani ushuru wa kusafirishia mazao ya uvuvi nje ya nchi katika mkoa wa Songwe kwa kigezo kuwa wote wanaziuza nje ya nchi,” amesema Ndaki.

Aidha, Waziri Ndaki amewataka wafanyabiashara hao kufanya biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na pia kuacha tabia ya kutorosha dagaa kwa kutumia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru, huku akiwaeleza kuwa endapo mfanyabiashara atakamatwa kwa kosa la utoroshaji dagaa atanyang’anywa leseni, mzigo wa dagaa pamoja na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Momba, Condester Sichalwe akiongea kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Ernest Silinde ambaye hakuwepo kwenye ziara hiyo, amesema kuwa suala la wafanyabiashara wa dagaa katika soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe kutozwa ushuru wa usafirishaji mazao ya uvuvi nje ya nchini (Export Loyalty) ni kero ya muda mrefu ambayo imekuwa ikiwaumiza wafanyabiashara hao pamoja na wananchi wanaonunua dagaa.