TEA kusimamia uanzishwaji na uhuishwaji wa Mfuko wa elimu

0
136

Miundombinu bora ya elimu katika halmashauri nyingi hapa nchini ni changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo.

Kauli hii imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bahati Geuzye, alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Amesema Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatambua umuhimu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika kuhamasisha na kuboresha mahusiano yao ya kiutendaji na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji kote nchini.

‘‘Kutokana na changamoto hizo za miundombinu bora ya elimu, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo inaratibu na kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeandaa utaratibu utakaowezesha halmashauri zetu kuanzisha Mifuko ya Elimu na kwa zile Halmashauri ambazo tayari zina mifuko hiyo tuna dhamira ya kuihuisha na kuanza kuitumia kikamilifu,’’ amesema Bahati.

‘‘Kazi iliyopo mbele yetu ni kutekeleza lengo kuu la kuanzisha na kuhuisha Mifuko ya Elimu katika hamlashauri zote nchini, moja ya mipango inayolenga uboreshaji wa elimu katika maeneo wanayoishi wananchi,’’ amebainisha Bahati