Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama tawala cha Msumbiji, FRELIMO, Roque Silva Samuel ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tano, ambapo katika mazungumzo hayo, viongozi hao pamoja na mambo mengine, wameeleza umuhimu wa kuendelea kulinda umoja, mshikamamo na udugu wa kihistoria uliopo kati ya vyama hivyo viwili.
Katibu Mkuu wa CCM ameeleza kuwa, Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mwenyekiti na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wataendelea kukuza ushirikiano wa kindugu uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji kwa nguvu zote, kwani nchi hizo mbili ni kama kaka na dada ambapo kamwe hawawezi kutenganishwa na kitu ama yeyote, na kutilia mkazo katika kuendelea kujenga muhimili wa uchumi.
Akieleza katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu wa FRELIMO amesisitiza kuwa CCM na FRELIMO ni vyama vyenye historia ya muda mrefu, kuanzia vita vya ukombozi, na mapambano hayo Tanzania ilikiwa msaada mkubwa.
Aidha, akiendelea kufafanua amesema, Tanzania iliteseka sana kuisadia FRELIMO na nchi nyingine katika ukombozi, hivyo kwa sasa FRELIMO na Msumbiji wanaiona Tanzania kama dunia ambayo wasingependa na hawapo tayari kuipoteza katika ushirikiano na mahusiano mazuri.
Katibu Mkuu wa FRELIMO amehitimisha kwa kusisitiza kuwa, Msumbiji na FRELIMO wataendelea kuwa pamoja na Tanzania kama ambavyo walikuwa pamoja katika mapambano mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kumuondoa Idd Amin Dada alipoivamia Tanzania.
Mazungungumzo hayo, yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Sekretarieti za Vyama vya CCM na FRELIMO ambapo kwa upande wa CCM ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, Katibu Wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ngemela Lubinga na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Hawasi Haule.