Ziwa Victoria kuchochea uchumi wa buluu

0
141

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali imejipanga kufanya mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.

Ulega amesema hayo alipotembelea eneo la kampuni ya kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa samaki kwa kutumika vizimba kandokando ya ziwa Victoria.

Amesema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili kupunguza muingiliano wa shughuli za ufugaji wa samaki na uvuvi wa asili ili shughuli zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.

“Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ufugaji wa vizimba unafanyika katika maeneo maalum na sio kila mahala… ili kutoa nafasi pia wavuvi wa asili waweze kuendelea na shughuli zao,” amesema Ulega.

Waziri Ulega amesema kuwa mpango huo utavutia wawekezaji wengi Ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, na hivi karibuni tumemuona akifanya jitihada kubwa kwa kuitangaza nchi yetu katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufungua milango ya uwekezaji, na moja ya maeneo ya uwekezaji aliyokuwa akiyatangaza ni katika uchumi wa buluu,” ameongeza Ulega