Bilioni 30 kujenga mtaa wa viwanda

0
168

Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amewataka Wakandarasi waliokabidhiwa kazi ya kujenga uzio wa mtaa wa viwanda na kituo cha kimataifa cha biashara Kurasini mkoani Dar es Salaam kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

Akizungumza baada ya utiaji saini mkataba baina ya uongozi wa Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji na Mauzo ya Nje (EPZA) na mshauri mwelekezi kampuni ya BICO pamoja na kukabidhi eneo kwa SUMA JKT, Profesa Mkumbo ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi huo kwa wakati ili Wawekezaji waliopatikana waanze kazi ya kujenga miundombini ya Kituo hicho mara moja.

Amesema shilingi bilioni 30 zimeidhinishwa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa ajili ya kujenga uzio wa eneo hilo la mradi, pamoja na kujenga miundombinu wezeshi.

“Kama mtakumbuka Mheshimiwa Rais aliagiza kujengwa kwa mitaa ya viwanda kama njia muhimu ya kuongeza uwekezaji wa viwanda na kuongeza mchango wa viwanda katika uchumi wa nchi, napenda kuwafahamisha kuwa huu utakuwa ni mtaa wa kwanza kujengwa nchini na hivyo ni utekelezaji kikamilifu wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan.” amesema Profesa Mkumbo