Serikali imetoa Shilingi milioni 700 kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 96 katika jimbo la Karagwe mkoani Kagera.
Pamoja na mambo mengine, ukarabati wa barabara hiyo utarahisisha mawasiliano, na kuboresha huduma za kijamii katika jimbo hilo la Karagwe.
Akiwa katika ziara yake ya kukagua barabara inayokarabatiwa kwa kutumia fedha hizo, Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametaka fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ukarabati wa barabara hiyo unaanzia kata ya Nyakahanga kwenda kata za Nyabiyonza, Bweranyange, Nyakakika, Nyakabanga, Kibondo na Lukanja.
Wakati wa ziara yake, Bashungwa alifuatana na Madiwani wa kata mbalimbali, Watendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Watendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).