Vikosi vya zimamoto mjini California nchini Marekani vinaendelea kufunika miti mikubwa katika msitu wa Taifa wa Sequoia ambao unateketea kwa moto.
Ndani ya hifadhi hiyo ndipo ulipo mti mkubwa na mrefu kuliko yote duniani, unaojulikana kama General Sherman.
Mti huo una urefu wa takribani mita 83 huku ukisadikiwa kuwa na miaka kati ya 2300 na 2700.
Miti mbalimbali pamoja na huo wa General Sherman ambao ni kivutio kikubwa cha utalii katika mji huo wa California, kwa sasa imefunikwa kwa utaalam mkubwa ili kuzuia athari zinazoweza kutokea endapo itashika moto.
Zaidi ya hekari milioni mbili zimeungua moto nchini Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja, huku chanzo kikuu cha moto huo kikitajwa kuwa ni mabadiliko ya hali ya hewa.
Mabadiliko hayo yanasababishwa na kuwepo kwa ukame unaoongeza joto, na hivyo kuruhusu mazingira ya kuwaka kwa moto msituni.