Washitiri wakutana kwa siku 5

0
144

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela amewataka Washitiri wa vipindi vya elimu kwa Umma kupata mafunzo ya teknolojia ya habari mara kwa mara, ili kufahamu mabadiliko ya sekta hiyo duniani kwa maslahi ya Taifa.

Mogela amesema hayo jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa 105 wa washitiri wa vipindi vya elimu kwa Umma na kuongeza kuwa, sekta ya habari ina nafasi muhimu ya kuelimisha umma kuhusu maendeleo ya nchi.

“Vyombo vya Habari vinaweza kutumika kujenga au kubomoa ajenda za nchi hasa ukiangalia ukuaji wa teknolojia ya habari ulimwengini, hivyo ni lazima wanahabari kujua nafasi yao katika kulinda maslahi ya Taifa hadi vizazi vijavyo.” amesena Mongela

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema ipo haja ya kutathmini namna mawasiliano yanavyoongeza thamani ya kazi zinazofanyika kila siku pamoja kuzungumzia umuhimu wa vyombo vya habari na mawasiliano katika maslahi ya Taifa.

Wadhamini wakuu wa mkutano huo ni Chuo kikuu cha Dar es Salaam ambapo Dkt. Dotto Kuhenga ambaye ni Mratibu wa Mawasiliano na Habari wa Chuo hicho amesema wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuisaidia jamii.

Washitiri wa vipindi vya elimu kwa Umma wanakutana kwa siku tano kwa lengo la kujengewa uwezo wa kutengeneza vipindi bora wakiongozwa na kauli mbiu – Vyombo vya Habari na Mawasiliano kwa Maslahi ya Taifa.