Mbowe na wenzake wakana mashtaka

0
195

 
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imepanga kuanza kusikiliza kwa mfululizo kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu tarehe 15 mwezi huu, baada ya washtakiwa kusomewa upya mashtaka yao na maelezo ya awali mbele ya Jaji Mustpha Siyani.
 
Hata hivyo washtakiwa hao wote wamekana mashtaka hayo yanayowakabili, lakini mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu ambao walikuwa askari, wamekiri kufanyakazi pamoja katika kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko mkoani Morogoro.
 
Washtakiwa hao wa kwanza hadi wa tatu ni Hassan Halfan Bwire, Hassan Kasekwa na Mohamed Lingenywa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Robert Kidando umeieleza mahakama hiyo kuwa watakuwa na mashahidi 24 akiwemo Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Boaz na baadhi Wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi za Airtel na Tigo.
 
Pia upande huo wa Jamhuri umetaja kuwa na vielelezo vya ushahidi ikiwemo vifaa vya JWTZ na JKT, bastola, Maganda mawili ya risasi na risasi moja.
 
Kwa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umesema utakuwa na mashahidi 11, ambapo 7 wamewekwa wazi  huku ukiomba mashahidi  wanne kutotajwa majina na nyadhifa zao kwa sasa kwa sababu za kiusalama na kulinda faragha zao.
 
Baada ya maelezo hayo Jaji Mustapha amekubaliana na hoja za Wakili Peter Kibatala na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 15 mwezi huu na washtakiwa hao wamerudishwa rumande.