Umoja wa Afrika (AU) umeismamisha uanachama nchi ya Guinea kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Jumapili iliyopita na kuipindua Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais Alpha Conde.
Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya yamelaaniwa na Jumuiya mbalimbali za Kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Kiuchumi Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo nayo imeisimamisha uanachama nchi hiyo.
AU imetangaza hatua hiyo baada ya ujumbe wake kutembelea Guinea ambapo ulikutana na uongozi wa kijeshi na kufanya mazungumzo ya kuutaka kurejesha utawala wa kiraia, kuwaachia huru Alpha Conde pamoja na mawaziri na maafisa wa Serikali iliyopinduliwa ambao wanashikiliwa kizuizini.
Katika utetezi wake uongozi wa kijeshi uliotwaa madaraka nchini Guinea umesema unataka kukomesha na kudhibiti vitendo vya rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa haki za binadamu.