Mahakama yatakiwa kutenda haki kwa wananchi

0
237

Watendaji wa mahakama nchini wametakiwa kujitoa katika kufanya kazi, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwaletea Wananchi maendeleo.

Kauli hiyo imeyolewa mkoani Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mathias Kabunduguru, wakati wa makabidhiano ya ofisi na Mtendaji Mkuu mpya wa mahakama nchini Profesa Elisante Ole Gabriel.

Kabunduguru amesema Watumishi wa umma ndio watunga sera, hivyo kuwataka kufanya kazi katika maeneo yao kwa kuzingatia haki na weledi, ili Wananchi wapate maendeleo yanayokusudiwa.

“Ninyi kama sehemu ya watunga sera wa umma mnategemewa kufanya kazi kwa haki, hivyo zingatieni hilo kwa moyo wa kujitoa ili mjenge Imani kwa jamii mnayoihudumia,” amesisitiza Kabunduguru

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel amesema kuwa, maslahi ya Watumishi na matumizi ya TEHAMA katika mahakama ni moja ya maeneo anayolenga kuyatafutia ufumbuzi baada ya kuanza majukumu yake rasmi akitokea wizara ya Mifugo na Uvuvi alipokuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo.

Aidha amewataka waandishi wa habari nchini kutumia kalamu zao vizuri kuhabarisha umma juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea mahakamani bila kupotosha.

“Waandishi wa habari tunawategemea katika kuhabarisha umma habari za kweli zisizoegemea upande wowote, hivyo fanyeni kazi kwa weledi ili jamii Ipate habari za uhakika.” amesema Profesa Ole Gabriel