Waziri Mkuu ataka usimamizi ujenzi mji wa Serikali

0
287

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu wasimamie kikamilifu awamu ya pili ya mpango wa ujenzi wa mji wa Serikali ulipo Mtumba jijini Dodoma ili ukamilike kwa wakati.
 
Ametoa agizo wakati akiongoza kikao kazi cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Katibu Wakuu pamoja na kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma.
 
Amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi huo, ambao utatekelezwa kwa awamu mbili kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023.
 
“Katika kufanikisha ujenzi huu ni vema tukahamasisha sekta binafsi kufanya uzalishaji ili kuweza kuwa na uhakika wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ikiwemo tofali, mchanga na kokoto.” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa
 
Amesema, baadhi ya wizara zimeanza taratibu za manunuzi na kuzitaka zile ambazo bado zihakikishe zinakamilisha utaratibu wa zabuni hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.