SERIKALI IMETOA MILIONI 500 KUJENGA KITUO CHA AFYA NARUNG’OMBE

Huduma za Afya

0
141

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 4, 2021 ameshirikiana na wananchi kusafisha eneo ambalo litajengwa kituo cha Afya katika Kata ya Narung’ombe, Ruangwa Mkoani Lindi.
 
Akizungumza na wananchi katika eneo hilo Waziri Mkuu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitahudumia wakazi wa Vijiji vya Nangurugai, Machang’nja, Chikwale, Chiundu, Liuguru, Itumbi, Nkoma na sehemu ya Chunyu
 
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameamua kuimarisha sekta ya afya kwa kuimarisha vituo vyote vya kutolea huduma, kituo hiki litawekwa eneo la kupokea wagonjwa na sehemu ya madaktari hadi watano kusikiliza wagonjwa”.
 
Amesema kuwa “Kutakuwa na maabara kubwa, jengo la mama na mtoto ikiwemo chumba cha upasuaji, kutakuwa na eneo la watoto njiti na kutakuwa na jengo kwa ajili ya upasuaji mdogo, wa kati na mkubwa”.
 
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kituo hicho, Rais Samia ameahidi kuwa atatoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ikiwemo vya  upasuaji na vipimo.