Zaidi ya watu milioni moja wanakabiliwa na njaa nchini Madagascar kufuatia ukame wa muda mrefu ulioikumba nchi hiyo.
Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa watu wengi wameripotiwa kula wadudu wakiwemo nzige, matunda na mizizi pori, kutokana na kukosa chakula.
Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema, dola milioni 75 za kimarekani zinahitajika ili kuwasaidia watu wanaokabiliwa na njaa nchini Madagascar kufuatia kukumbwa na ukame huo.
Idadi kubwa ya watoto na wazee wanakabiliwa na utapiamlo kufuatia ukame huo, ambao unaelezwa kuwa ni mbaya zaidi kuikumba Madagascar katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.