EWURA yasitisha bei mpya za mafuta

0
3519

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kusitisha bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika leo Septemba 1, 2021 na kuagiza bei za mwezi uliopita kuendelea kutumika.

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma na kusema uamuzi huo umetokana na maelekezo ya serikali ambayo inafanya mapitio ya upangaji wa bei na viashiria vinavyopelekea kupanda kwa bei ya mafuta nchini.

“Bei zilionekana zinapanda, na baada ya kutoa matangazo hayo, tumepata maelekezo mahususi kutoka serikalini kwamba bei hizo zisitishwe na tuendelea kutumia bei zilizokuwa zinatumika mwezi uliopita,” amesema Chibulunje.

Ameeleza kuwa bei za zamani zitaendelea kutumia hadi hapo mapitio hayo yatakapokamilika, na kwamba watawaeleza Watanzania majibu ya uchunguzi.

Timu hiyo inajumuisha watu kutoka wizara ya fedha, wizara ya nishati, Mamlaka ya Mapato Tanzania, EWURA, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na taasisi nyingine za serikali.

Taarifa ya EWURA jana ilieleza kwa Septemba 2021 bei za rejareja za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kwa shilingi 84/Lita, Shilingi 39/lita na Shilingi 18/lita, mtawalia. Vilevile bei za jumla za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka, Shilingi 39.05/lita na Shilingi 18.05/lita , mtawalia.