MWENGE KUZINDUA MIRADI 13 TANDAHIMBA

0
178

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya amekabidhi Mwenge wa Uhuru 2021 kwa Mkuu wa Wilaya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala baada ya mwenge huo kukimbizwa katika wilaya hiyo na kukagua, kuona na kuzindua miradi minane ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.1.

Akiongea baada ya kuupokea mwenge huo, Kanali Sawala amesema utakimbizwa kwenye njia ya urefu wa kilomita 76.5 katika Wilaya ya Tandahimba kukagua, kuona na kuzindua miradi 13 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8.

Baadhi ya miradi itakayopitiwa ni pamoja na Zahanati ya Miuta ambayo itazinduliwa, Hospitali ya Wilaya kuona na kupata taarifa ya wilaya kuhusu matumizi ya TEHAMA. Miradi mingine ni uwekaji wa jiwe la Msingi Ujenzi wa Benki ya PBZ, ukaguzi na kuweka jiwe la Msingi Ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho cha JABARI

Mwenge wa Uhuru 2021 ulipokelewa mkoani Mtwara jana kutoka mkoa wa Lindi ambapo umepitia jumla ya miradi 42 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.1.