Serikali kuendelea kushirikiana na sekta Binafsi katika kutoa Elimu bora

0
194

Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta ya elimu ila hata sekta binafsi zilizopo kwenye sekta hiyo zitoe elimu bora kwa watanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufindi stadi, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa anazungumza na wananchi katika shule ya msingi ya Mtakatifu Dominica iliyopo Mkoani Iringa.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufindi, Profesa Joyce Ndalichako alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Upadri kwa muasisi wa shule binafsi za msingi mkoani Iringa, Padri Aidan Ulungi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kitaaluma kimkoa na kitaifa.

Profesa Ndalichako amesema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika elimu na kuzitaka kutoa elimu inayoambatana na ujuzi, na uzalendo wa kuipenda nchi yao.

Katika taarifa yake kwa Waziri, Mkurugenzi wa Shule za Mtakatifu Dominica, Padre Aidan Ulungi ameishukuru serikali kwa kuendelea kuziunga mkono shule binafsi kwa kuwa pamoja na kutoa elimu bora pia zinatoa ajira nyingi za walimu.

Awali Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Iringa, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa amempongeza Mkurugenzi na muasisi wa shule hizo ambazo zinahudumia wananchi wengi wa ndani nan je ya mkoa.

Padri Ulungi aliyetokea kuwa mvuvi, kisha mfanyakazi wa ndani na baadae kujiongeza na kujiendeleza kielimu katika mazingira magumu, amewezesha Kanisa hilo kumiliki shule saba za msingi na sekondari, kituo cha afya na kuajiri wafanyakazi 400.