Emmaule Samwel, TBC Dar es Salaam
Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mahakama nchini imetajwa kuwa nyenzo muhimu itakayorahisisha utaoji huduma kwa wakati kwa wananchi wanaotafuta haki zao mahakamani.
Hayo na Mtendaji Mkuu wa Mahamaka, Profesa Elisante Ole Gabriel mara baada ya kujitambulisha rasmi kwa watendaji wa mahakama nchini kwenye kikao cha ndani ambacho kimeendeshwa kwa njia ya video conference.
“TEHAMA imesadia kwa kiasi kikubwa kupunguza baadhi ya changamoto za mashauri mahakamani hivyo tutaendelea kuboresha mfumo wa TEHAMA eneo la mahakama ili upatikanaji haki uwe kwa wakati,” amesema.
Pamoja na mambo mengine mtendaji huyo amewataka watendaji wa mahakama wananchi na viongozi wa dini wanaotafuta haki kuwa mstari mbele kupiga vita rushwa ambayo ni adui wa haki kwenye jamii.
“Lazima tuimarishe mifumo yetu ya kimahakama kwa kuhakikisha watendaji hawapokei rushwa, lakini pia wateja wetu nao wasiweze kushawishi watendaji kula rushwa,”amesisitiza Ole Gabriel.
Prof. Ole Gabriel ameanza kazi rasmi ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kushika jukumu hilo akitokea Wizara ya Mifugo na Uvuvi alipokuwa katibu mkuu.