Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde limewasimamisha kazi Wachungaji 17 kwa madai ya kukiuka maadili ya kikristo na wito wa kichungaji wa kanisa hilo.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Mbeya, Katibu Mkuu wa KKKT wa Dayosisi hiyo Mchungaji Ikupilika Mwakisimba amesema wachungaji hao wamekuwa wakipinga na kuhamasisha Makao makuu ya Dayosisi kuendelea kuwa Tukuyu badala ya jijini Mbeya.
Amesema wachungaji hao waliamua kutangaza uasi kwa kukataa maelekezo ya Askofu wa KKKT Dayosisi ya Konde Dkt. Edward Mwaikali pamoja na kuandika waraka wa kutokua na imani na Askofu huyo pamoja halmashauri kuu ya Dayosisi hiyo.
Kwa upande wake Askofu Dkt. Mwaikali amesema uongozi wa kanisa hilo ulijaribu kuwaelimisha Wachungaji hao juu ya athari za kuchanganya masuala ya utumishi na mambo ya itikadi za kisiasa na kuwaita kwa mazungumzo lakini imeshindikana.
Kufuatia mgogoro uliopo Dkt. Mwaikali amesema halmashauri kuu ya KKKT Dayosisi ya Konde inatarajia kukaa na pande zote ambazo zinavutana juu ya kuhamisha Makao makuu ya Dayosisi ya Konde kutoka Tukuyu wilayani Rungwe na kwenda usharika wa Ruanda jijini Mbeya.