Akamatwa akiwauzia wananchi dawa zilizokwisha muda

0
286

Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi (TMDA), Nyanda za Juu Kusini imekamata shehena ya dawa zilizokwisha muda wake katika nyumba ya mkazi mmoja wa Igawilo jijini Mbeya.

Shehena hiyo ya dawa yenye thamani ya shilingi milioni 7.7 imekatwa na TMDA kwa kushirikiana na jeshi la polisi baada ya kufanya upekuzi kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa TMDA, Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwepo kwa mtu huyo ambaye amepakia shehena ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika nyumba yake huku akiendelea kuuza licha ya muda wake kuisha, na akitumia mihuri na vifaa vingine kubadilisha ili zionekane hazijaisha muda wake.

Amesema dawa na vifaa tiba walivyovikamata kuwa ni antibayotiki, sindano na nyuzi za kushonea, malaria na asidi ambazo ni za serikali zikiwa zimefutwa lebo.

“Dawa zote zimekutwa katika makazi ya mtu zikiwa zimewekwa katika hali isiyofaa bila mpangilio wowote kinyume cha sheria ya dawa ya vifaa tiba na sheria ya nchi sura ya 219 ya mwaka 2013 kwa sababu vitu vilivyokutwa ni mali ya serikali, tumeorodhesha dawa zote na zimechukuliwa, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya utaratibu mwingine,” amesema Mshighati.

Aidha, amesema wanaendelea kudhibiti mpaka wa Tunduma na Kasumulu ili dawa za magendo na zilizokwisha muda wake zisiingizwe nchini huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuepukana na athari za kiafya.

Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanyanje, Nessy Shitambala ameeleza kusikitishwa na tukio la mwananchi wake kukutwa na shehena ya dawa nyumbani kwake mali ya serikali ambayo zimekwisha muda wake.