24 kutoa ushahidi kesi ya Mbowe

0
216

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali Mwanadamizi Nassoro Katuge katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demeokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Freeman Mbowe na Wenzake watatu, umewasilisha maelezo ya mashahidi 24 na vielelezo vitakavyotumika kama ushahidi wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa katika mahakama kuu kitengo cha mafisadi.

Vielelezo hivyo pamoja na maelezo ya mashahidi yamewasilishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo kwa dharura na kusomewa upya mashtaka yao yanayowakabili.

Katika moja ya vielelezo vilivyowasilishwa, mshtakiwa Mbowe anadaiwa kula njama ya kuwadhuru Viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya.

Pia katika kielelezo kingine inaelezwa kuwa mshtakiwa Mbowe katika tarehe tofauti mwaka mwaka 2020 na 2021 alimpigia simu  Luteni David Urio ili  wakutane ofisini kwake  Kinondoni mkoani Dar es Salaam  kwa lengo la kumpa kazi ya kumtafutia  Wanajeshi wastaafu, makomandoo na wale waliofukuzwa jeshini ili kumsaidia kuchukua dola.

Upande utetezi ukiwakilishwa na wakili Peter Kibatala umeieleza mahakama hiyo kuwa watakuwa na mashahidi wengi akiwemo  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini  Simon Siro na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya.

Agosti 17 mwaka huu, Mahakama Kuu kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi ilipokea taarifa katika Mahakama ya Kisutu kwamba Mbowe na wenzake wapelekwe mahakamani hapo wasomewe mashitaka yao na maelezo ya mashahidi, ili kesi hiyo ihamie mahakama ya uhujumu uchumi.

Baada ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vyake, washtakiwa wamepelekwa rumande mpaka hapo Mahakama Kuu kitengo cha mafisadi itakapotoa taarifa rasmi juu ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.