Miongoni mwa utalii unaokuwa kwa kasi nchini ni utalii wa mikutano. Pengine huenda ukawa unajiuliza utalii wa mikutano (MICE) ni nini?
Kama ilivyo kawaida kwa watu mbalimbali duniani kufunga safari kwa ajili ya kutembelea vivutio vilivyopo maeneo tofauti kwa ajili ya kujifunza na kuburudika, hivyo Bodi ya Utalii nchini (TTB) kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), imeandaa mpango maalumu wa watalii kufanya mikutano ndani ya nchi kisha kutembelea vivutio.
Mpaka sasa Bodi ya Utalii imetembelea baadhi ya mikoa nchini kujionea mazingira ya kupokea watalii pamoja na kuchukua maoni kwa wadau wa utalii ikiwemo wamiliki wa Hoteli, Wakulima wa zabibu na watengenezaji wa mvinyo ili kuweka njia bora ya kukuza aina hiyo ya utalii.
Lilian Fungamtama ni Kaimu Meneja wa Mikutano na Matukio kutoka Bodi ya Utalii nchini, amesema kwa maeneo ambayo wamekagua yanaridhisha kufanyika kwa mikutano hivyo wadau wachangamkie fursa hiyo ya utalii wa mikutano.
“Tumedhamiria kukuza utalii na njia mojawapo ya kukuza ni kuongeza njia mbalimbali za kuwaalika watalii nchini, lakini utalii huu sio kwa ajili ya watu kutoka nje pekee bali hata wa ndani ya nchi wanaweza kuandaa mikutano yao ambapo sisi tutawaelekeza mahali sahihi pa kutumia ndio maana tumeona tukague na tujue idadi ya watu watakaokuwa na uhitaji, sisi tayari tunakuwa na taarifa za sehemu hiyo”-amesema Lilian.
Maeneo yaliyofanyiwa ukaguzi ni pamoja na Zanzibar, Dodoma, Mwanza na Mara ambapo maeneo yanayotarajiwa kufanyika ukaguzi ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam.