Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza wanariadha watatu wa Tanzania walioshiriki mashindano Olimpiki ya Tokyo 2020 na kuwataka viongozi wa kamati ya Olimpiki Tanzania kuongeza nguvu katika kuibua vipaji.
Rais ametoa pongezi hizo Ikulu Jijini Dar es salaam, wakati wa hafla maalumu aliyowaandalia wachezaji wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 baada ya kuibukna mabingwa wa michuano ya CECAFA na washiriki wa michuano ya Olimpiki.
Rais Samia amesema “Kwa Taifa kubwa kama letu, kuwakilishwa na watu wachache ni aibu…turekebishe kule mbele.”
Ameongeza kuwa viongozi wajipange na wawe na mikakati mizuri ya kukuza michezo nchini ili kuwe na washiriki wengi zaidi siku zijazo zijazo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Kamati la Olimpiki Tanzania (TOC) Henry Tandau amekiri kuwepo kwa uhaba wa washiriki na kupendekeza mambo yatakayosaidia kukuza ushiriki ikiwemo maboresho ya miundombinu ya michezo.
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameahidi kufanya kila linalowezekana kurudisha ushindi nyumbani.
“Tukuhakikishie [Rais Samia] zile heshima za mwaka 1980 ambazo akina Filbert Bayi na Nyambui walileta medali, tunakuhakikishia timu hii iliyopo mbele yako tutashirikiana kurudisha heshima ya nchi yetu,” amesema Bashungwa.