Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuwa kituo cha kibiashara kinachotoa taarifa, takwimu sahihi na huduma bora za kibiashara ndani na nje ya nchi ili kukuza na kuendeleza Biashara nchini.
Waziri Mkumbo aliyasema hayo katika hafla fupi ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANTRADE iliyofanyika katika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Nkoani Dar es salaam.
Akizindua Bodi hiyo, Profesa Mkumbo ameitaka bodi hiyo kusimamia ipasavyo majukumu muhimu ya TANTRADE ikiwemo kuanzisha kanzi data yenye taarifa za kibiashara na kufanya utafiti ili kujua ni bidhaa gani zinazalishwa kwa wingi nchini, kuna upungufu wa bidhaa gani na bidhaa gani zinahitajika zaidi nje ya nchi.
“ Nataka kuona TANTRADE inakuwa kimbilio kwa wanyabiashara katika kuwaunganisha wazalishaji, wasindikaji wafanyabiashara kutoka maeneo ya uzalishaji na walipo wtateja wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi kwa kutoa taarifa na takwimu sahihi pamoja na huduma bora za kibiashara”. Amesema Waziri Mkumbo.
Waziri Mkumbo pia ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha TANTRADE inaongeza ubunifu katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya kimtandao ya biashara inayolenga kuongeza upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kibiashara kwa urahisi ili kuwezesha upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.
Aidha, Profesa Mkumbo ameielekeza Bodi hiyo kutekeleza jukumu la msingi la Bodi katika kutengeneza mkakati wa kufikia malengo ya Taasisi na kusimamia utekelezaji wake kwa kutoa ushauri ndani na nje ya vikao vya Bodi.