Mara: RC Hapi akerwa kukosekana choo cha abiria

0
158

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi ametoa mwezi mmoja kwa TEMESA mkoani Mara kujenga eneo la mapumziko pamoja na choo kwa abiria wanaotumia kivuko cha MV Musoma katika eneo la Mwigobero katika Manispaa ya Musoma.

Hapi ametoa agizo hilo baada ya kutembelea kivuko hicho na kisha kupokea kero za abiria ambapo walimweleza kuwa, wamekuwa wakipata tabu kwa kukosa eneo la mapumziko wakati wakisubiri kivuko.

Waliongeza kuwa hata nyakati za mvua wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata maeneo ya kujikinga hali inayowafanya wasafiri wakiwa wameloana.

Hapi amesema inasikitisha kuona abiria wanapata tabu kwa kiwango hicho huku lengo la Serikali ikiwa ni kutoa pamoja na kuboresha huduma mbalimbali katika maeneo hayo.

Hapi amesema Kivuko hicho kimeanza kazi muda mrefu hivyo ni ajabu kukosa choo na jengo la mapumziko huku wahusika wakiendelea kutozwa tozo mbalimbali katika eneo.

Kivuko cha MV Musoma kinafanya safari zake kati ya Manispaa ya Musoma na Rorya mkoani Mara ambapo kina uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 250